Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia siku ya pili tukiwa kwenye makazi mapya ambapo ghafla alitokea paka mweusi mwenye sura ya binadamu na kusimama mlangoni. Je, paka huyo atafanyaje? Tuwe pamoja.
Yule paka mwenye sura ya kibinadamu aliendelea kusimama kwa muda mrefu bila kunisemesha jambo lolote kisha akaondoka zake.Kesho yake, mama mmoja alinifuata na kunilaumu kwa nini tulihamia kwenye nyumba ile bila kuwauliza majirani.
Nilipomuuliza sababu za kuniambia hivyo alisema ile nyumba haikuwa nzuri na kwamba hakuna mpangaji aliyekuwa akimaliza miezi sita tangu ahamie.“Mmefanya makosa kuhamia bila kuwauliza majirani, nyumba hiyo pamoja na uzuri wake haifai, watu huwa wanakimbia na kuacha vitu vyao,” Stumai alimkariri mama huyo.
Baada ya kuniambia hivyo nilichoka lakini sikuwa na la kufanya kwa sababu fedha tuliyokuwanayo ndiyo tulilipa kodi, nilipomwambia mume wangu naye alichoka.
Siku ya pili tukiwa katika makazi hayo mapya, mama mwenye nyumba hiyo aliyekuwa kikongwe wa miaka kama 80 ambaye pia alikuwa akiishi na mama yake aliyekuwa na miaka kama 100 aliniita na kuniambia hatukutakiwa kwenda msalani baada ya saa sita mchana.
Sharti hilo lilikuwa gumu sana, nikamuuliza kwa nini hakuliweka kwenye mkataba wa kupangishiana nyumba akaniambia ndiyo hivyo, tukikiuka kitachotupata tusimlaumu.Kwa kuwa aliponiambia hivyo mume wangu hakuwepo aliporejea jioni nilimwambia naye akashangazwa na sharti hilo na kunieleza tangu alipoanza kupanga nyumba hakuwahi kukutana na jambo kama hilo.
“Tangu nilipoanza kupanga nyumba hii itakuwa ya nne, sijawahi kukumbana na masharti kama ya hapa, hawa akina bibi watakuwa washirikina tu!” Stumai anasema mumewe alimwambia.Kama nilivyokuambia kwamba kwa kipindi hicho hatukuwa na fedha kabisa, hivyo nilimweleza mume wangu kwamba tutakaa pale na hatukupaswa kuogopa chochote.
Siku moja tukiwa tumekaa pale kama siku sita huku tukifuata lile sharti la kutokwenda msalani baada ya saa sita mchana, kwenye saa saba usiku nilibanwa na tumbo la kuendesha.Tumbo hilo halikuwa la kawaida ndipo nilimuomba mume wangu anisindikize msalani, wote tulisahau kabisa lile sharti tulilopewa, tukiwa nje ya nyumba mume wangu alibaki nje kunisubiri mimi nikiwa msalani.
Baada ya kuketi na kuanza kujisaidia, katika hali ya kustaajabisha nilimuona mtu akija kwa kasi usawa wa mlango, nikawa najiuliza nilikuwa naota au ilikuwa hali halisi!Wakati mtu huyo mwenye jinsi ya kiume akizidi kuja kwa kasi nikasikia sauti ikiniambia nisipige kelele bali nitulie kimya, licha ya mwili kunitetemeka na nywele kunisisimka, nikatulia na kuendelea kumwangalia mtu huyo.
Licha ya mtu huyo kuwa na macho makali, nilimuangalia kwa makini ndipo aliingia mle chooni na kusimama nyuma ya mlango ambao ulikuwa wa mabati.Kitendo hicho kiliniogopesha sana ila sikuthubutu kupiga kelele, kwa hofu niliyokuwanayo nilitamani kutoka mle ndani bila hata ya kunawa lakini kitendo bila kuchelewa, nilijikuta nimebeba ndoo ya maji na kujimwangia mwilini.
Baada ya kufanya hivyo, nilitoka mle ndani kwa kasi lakini nikiwa nimepiga hatua tatu nilianguka na kupoteza fahamu, nilipozinduka nilijikuta nikiwa chumbani kwetu.“Stumai umepatwa na nini mke wangu?” Mumewe alimwuliza.
Kwa kuwa sikutaka kumpa hofu, nilimdanganya kwamba nilihisi kizunguzungu ndipo aliniambia twende hospitali nikamwambia asijali kwa muda ule nilikuwa najisikia vizuri sana.Baada ya kutulia na kuanza kutafakari juu ya tukio lile la kutisha, nikakumbuka nilikuwa nimekiuka masharti ya kutoingia chooni baada ya saa sita.
Licha ya kukumbuka hivyo, sikutaka kumweleza mume wangu tukalala, kulipokucha mume wangu alinijulia hali na kuniuliza niliendeleaje nikamwambia vizuri.Kwa kuwa nilimhakikishia kwamba hali yangu ilikuwa nzuri, aliniaga akaenda kibaruani nami nikabaki na mwanangu.
Nilipoamka mtu wa kwanza kukutana naye alikuwa mama mwenye nyumba ambaye alinifuata, aliniamkia na kunipa hongera kwamba nilionekana mtoto lakini nilikuwa mtu mkubwa.Kufuatia kauli yake nilimuuliza sababu za kuniambia hivyo, bila soni akaniambia kama ningepiga kelele mle chooni muda ule ningekuwa maiti.
“Wewe mtoto ni mzito sana, watu wakikuangalia wanaweza kukuona ni mtoto mdogo kumbe ni mkubwa yaani ungepokea simu ulikuwa umekwisha,” Stumai anasema mama mwenye nyumba alimwambia.Aliponieleza hivyo, moja kwa moja nilibaini yule mtu alikuwa jini na ilikuwa animalize sema kilichonisaidia ni kutii sauti iliyonizuia nisipige kelele.
Pia nilibaini kwamba kule chooni yalikuwa makazi ya majini wake ambao walikuwa wakirudi saa sita kutoka alikokuwa anawatuma ndiyo maana alituzuia kwenda huko baada ya muda huo.Kwa kuwa nilikuwa ninajiamini, niliapa kuendelea kukaa pale na kujisemea moyoni kwamba sitapatwa na balaa lolote mpaka tutakapohama wenyewe.
Baada ya bibi kujidhihirisha wazi kwamba ndiye aliyetaka kuniondoa duniani aliendelea na mambo yake lakini kama nilivyokuambia kwamba wachawi huwa hawakati tamaa aliamua kula sahani moja na mimi.Kuanzia siku hiyo visa vikaongezeka usiku na mchana kwani yule bibi alikuwa akijigeuza viumbe vya ajabu na kuingia chumbani kwetu, kukaa nje ya mlango au juu ya bati.
Miongoni mwa tukio lililoniacha hoi lilitokea usiku wa manane tukiwa tumelala, niliposhtuka usingizini sikumuona mwanangu ambaye alikuwa akijifunza kukaa.Kwa kuwa alikuwa amelala katikati nilimuamsha mume wangu na kumweleza mtoto hakuwepo, kweli alipogundua hakuwepo licha ya chandarua kuwa kama tulivyokichomeka kitandani alitaharuki.
Nilikurupuka pale kitandani, nilipigwa na butwaa kumuona mtoto wetu ambaye hakuwa na uwezo wa kushuka kitandani peke yake, akiwa ameketi amenyanyua mguu kauweka kinywani huku akiulamba.Nilimwinua haraka na kuanza kumchunguza, nikabaini alikuwa salama, nikamwambia mume wangu ilikuwa kazi ya yule mama akaniuliza tufanyeje, nikamwambia atulie tu!
Baada ya kukaa wiki mbili, siku moja nikiwa nimeketi nje ya nyumba nilitupia macho juu ya banda la mkaa la yule bibi nilimuona paka mkubwa mweusi ambaye sura ilikuwa ya yule mama mwenye nyumba.


Post a Comment